Chanzo kutoka Israel kimeiambia Sky News Arabia kwamba wapiganaji 50 wa kundi la Hezbollah walikuwepo kwenye kituo cha amri na udhibiti (command and control complex) katika safu ya milima ya Ali Tahr wakati kilipolipuliwa, na wengi wao waliuawa. Kituo hicho kimekuwa kikifanya kazi kwa siri chini ya ardhi kwa miaka mingi.
Chanzo hicho kimesema kuwa Israel haina mpango wa kuondoa majeshi yake kwenye safu hiyo ya milima, bali itapanga upya vikosi vyake vya jeshi (IDF) katika eneo hilo, ambavyo vitashambulia mara moja mtu yeyote atakayesogelea eneo hilo lililolipuliwa.
Chanzo hicho kilikanusha vikali uwepo wa Wairani wowote ndani ya kituo hicho na kusema kuwa jeshi la IDF lilikuta shehena kubwa ya silaha hapo.
Kituo cha amri na udhibiti ndio ubongo wa operesheni za kijeshi. Hapo ndipo mipango inapangwa na mawasiliano yanapofanyika. Kupoteza kituo ambacho kilijengwa na kufichwa chini ya ardhi kwa miaka mingi, pamoja na kupoteza wapiganaji wengi kwa mpigo, ni pigo kubwa linalodhoofisha uwezo wa kundi hilo kuratibu mashambulizi kutoka eneo hilo.
Katika vita, anayeshikilia milima ndiye anayemiliki uwanja wa mapambano. Uamuzi wa Israel wa kutoondoka kwenye milima ya Ali Tahr unaonyesha nia yao ya kumiliki miinuko hii ili kuwa na uwezo wa kuona mbali (surveillance) na kuzuia Hezbollah wasirudi kusogeza silaha au kujenga upya ngome zao karibu.
Sehemu inayovutia zaidi ni Israel kukanusha vikali kwamba hapakuwa na Wairani. Katika siasa za Mashariki ya Kati, Iran inaiunga mkono Hezbollah. Ikiwa Israel ingesema imewaua Wairani (kama makamanda wa IRGC), ingeilazimu Iran kujibu mapigo ili kulinda heshima yake. Kukanusha huku kunaweza kuwa ni mbinu ya Israel ya kuepuka kupanua wigo wa vita na badala yake kuifanya ibaki kuwa ni ishu ya Israel dhidi ya Hezbollah pekee.
Kwa kusisitiza kwamba walikuta shehena kubwa ya silaha, jeshi la Israel (IDF) linatuma ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa kuhalalisha uharibifu wa kituo hicho, likionyesha kuwa hilo lilikuwa shabaha halali ya kijeshi (legitimate military target).
