IRAN YAPANUA VIZUIZI VYA MAJINI: Yaweka Sheria Mpya Lango la Hormuz, Marekani Yapinga!



Iran inajiandaa kuanzisha eneo jipya la vizuizi  la majini katika Ghuba ya Uajemi, kuanzia eneo la sasa la mzingiro wa Marekani hadi Lango la Hormuz, kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa Iran, Mohsen Rezaei.

Tehran inasema pia itachapisha ramani mpya kwa ajili ya njia za meli kupitia Lango la Hormuz na imetoa onyo kali kuwa meli yoyote itakayoingia kwenye eneo hilo lililozuiliwa bila ruhusa ya Iran, inaweza kukabiliwa na vikwazo vikali.

Onyo hili linakuja muda mfupi baada ya Iran kusema imefanyia majaribio kombora lake la balestiki aina ya Qassem Basir dhidi ya manowari ya Marekani, ikionyesha kwa vitendo kuwa vikosi vya majini vya Marekani vinavyofanya doria karibu na Hormuz viko ndani ya masafa ya shabaha ya Tehran. Marekani imekataa na kupinga vikali jaribio hilo la Iran la kuweka eneo lake la vizuizi.

Iran haipingi mzingiro wa Marekani kwa kutumia nguvu za kijeshi pekee, bali sasa inajaribu kuweka sheria zake yenyewe za kudhibiti usafiri wa majini kuzunguka Lango la Hormuz.

Hali hii inaweza kugeuza lango hili muhimu zaidi duniani la kupitisha mafuta kuwa uwanja wa mashindano ya moja kwa moja ya kuwania udhibiti kati ya Washington na Tehran.

Kwa kutangaza eneo la vizuizi na kuchora ramani mpya, Iran inajaribu kuhalalisha udhibiti wake kisheria. Hii inamaanisha wakiipiga meli yoyote ya kibiashara au ya kivita ya Marekani, watajitetea kimataifa kuwa meli hiyo ilivuka mipaka na kuingia eneo lao bila ruhusa. Ni mbinu ya kujiwekea kinga ya kidiplomasia.

Marekani imesema imekataa sheria hizo za Iran. Lakini kukataa kwa mdomo hakutoshi. Kama meli za Marekani zitaendelea kupita na Iran ikazishambulia kwa makombora kama Qassem Basir, Marekani itabidi ijibu kwa nguvu zote au isalimu amri na kukwepa eneo hilo. Hili ni jaribio la wazi la kupima ujasiri wa Washington.

Lango la Hormuz ndio njia kuu inayopitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa kwa njia ya bahari duniani. Mashindano haya ya nani anadhibiti njia yatafanya kampuni kubwa za bima zipandishe gharama za bima kwa meli, jambo litakalopandisha bei ya mafuta ghafla katika soko la dunia. Athari hii itafika hadi kwenye vituo vya mafuta na masoko ya bidhaa hapa Afrika.

Post a Comment

Previous Post Next Post