MOTO UNASAMBAA KWA KASI! IRAN SASA YAIVAA KOREA KUSINI NA KUTOA ONYO LA KUTISHA!



Wakati dunia ikiwa bado imeshikilia pumzi kutokana na mivutano mikali kati ya Marekani na Iran katika Lango la Hormuz, serikali ya Tehran imepanua wigo wa vitisho vyake na sasa imeigeukia Korea Kusini. Iran imetoa onyo zito na la wazi kwa serikali ya Seoul ikitahadharisha kuhusu madhara makubwa endapo taifa hilo la Asia litapeleka vikosi vyake au kushiriki katika operesheni zozote za kijeshi ndani ya Ghuba ya Uajemi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka serikali ya Iran, ushiriki wowote wa kijeshi wa Korea Kusini katika eneo hilo, utachukuliwa moja kwa moja kama kitendo cha kuiunga mkono Marekani dhidi ya Iran, na hivyo kuifanya Korea Kusini kuwa adui halali kwenye uwanja wa vita.

Akizungumza kwa msisitizo mkubwa, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baghaei, aliitaka Korea Kusini kujiepusha na shinikizo la Marekani. Alinukuliwa akisema:

"Hakuna taifa huru na linalowajibika linalopaswa kusalimu amri chini ya shinikizo na vitisho vya Marekani na kuwa mshirika katika vitendo vya uchokozi na uhalifu wa kutisha dhidi ya taifa kuu la Iran".

Kauli hii ni ujumbe wa moja kwa moja kuwa Iran haitavumilia kuona nchi washirika wa Marekani wakitumika kuongeza nguvu ya kizuizi cha majini  kinachoendelea kuiandama nchi hiyo kiuchumi.


Ili kuelewa kwa nini Korea Kusini inajikuta katikati ya moto huu, lazima tuangalie mambo mawili makuu: Uchumi na Ushirika wa Kijeshi.

1. Utegemezi wa Mafuta (Nishati):Korea Kusini ni miongoni mwa mataifa yaliyoendelea sana kiviwanda barani Asia, lakini haina mafuta yake yenyewe. Inategemea sana mafuta ghafi kutoka Mashariki ya Kati, na kiasi kikubwa cha mafuta hayo hupitia kwenye Lango la Hormuz. Hivyo, usalama wa lango hilo ni suala la uhai au kifo kwa uchumi wa Korea Kusini.

2. Shinikizo Kutoka Marekani: Marekani, ambayo ni mshirika mkuu wa kijeshi wa Korea Kusini (ikiilinda dhidi ya Korea Kaskazini), imekuwa ikizishinikiza nchi washirika wake duniani kuchangia nguvu za kijeshi na manowari zao ili kulinda meli za kibiashara zinazopita kwenye lango hilo, mbinu inayoitwa Burden Sharing (Kugawana mzigo wa kiulinzi).

Vitisho hivi vinaweka serikali ya Seoul katika njia panda ngumu sana kijiopolitiki. Ikiwa Korea Kusini itapeleka vikosi, inajiweka kwenye hatari ya mashambulizi ya moja kwa moja kutoka kwa makombora ya Iran au mabomu ya majini. Iran imeonyesha uwezo wake wa kushambulia na kutaifisha meli za mafuta zinazomilikiwa na nchi zinazoipinga.

Kushambuliwa kwa meli za Korea Kusini kutasababisha mtikisiko mkubwa sio tu kwa nchi hiyo, bali kwa masoko ya kifedha na nishati barani Asia yote. Kwa upande mwingine, ikiwa Korea Kusini itakataa kuiunga mkono Marekani, inaweza kudhoofisha uhusiano wake wa kiusalama na Washington, jambo ambalo ni hatari kwao hasa ukizingatia vitisho vya nyuklia wanavyovipata kila siku kutoka kwa jirani yao, Korea Kaskazini.

Sakata hili linazidi kudhibitisha kuwa mgogoro wa Ghuba sio tena suala la Marekani na Iran pekee, bali ni bomu linalosubiri kulipuka na kuivuta dunia nzima kwenye vita vya kiuchumi na kijeshi.

Endelea kufuatilia Swahili Prime Media kwa uchambuzi wa kina na habari za usalama wa kimataifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post